Saturday, September 22, 2012

Super Sunday imewadia-Liverpool vs Manchester United

Nadhani wadau hakuna siku ambayo washabiki wa mpira duniani watakua makini kufuatilia mpira na kutopepesuka katika kuangalia kama leo.Na nadhani hakuna mahali duniani ambapo kuna mechi zenye mvuto na zinazoweza kuvuta hisia za watu kama mechi itakayochezwa leo kule Anfield kati ya Liverpool ambao ni wenyeji dhidi ya Manchester United ambao ni wapinzani wao wa jadi kwa miaka mingi.Upinzani wa jadi unaohusishwa na malumbano pamoja na utani kuhusu mafanikio kati ya timu hizo unaosemekana kuchochewa sana na mashabiki wa Liverpool kujigamba sana kuhusu mafanikio ya timu yao miaka ya 80 ambapo walikua wakifanya vizuri sana kwenye ligi ya Uingereza na pia Ulaya na hivyo kujisimika kama timu bora nchini humo na mojawapo ya miamba ya soka barani Ulaya,heshima ambazo Liverpool kwa ushahidi wa vikombe vyake wapo sahihi kujigamba nazo.
Miaka ya karibuni Manchester United wametokea kuwa na matokeo yenye tija zaidi wakibeba vikombe lukuki katika mashindano mbalimbali na kadiri siku zinavyokwenda wameweza kufuta gepu la vikombe na kuwafikia Liverpool kwa vikombe vya ligi kuu ya Uingereza,yaani kushinda mara 19 lakini bado hawajaweza kuwafikia kwa namba ya vikombe katika bara la Ulaya.Leo hii timu hizi zinakutana kukiwa ni siku maalum ya kumbukumbu kwa mashabiki wa Liverpool waliokufa huko Hillsborough mwaka 1989 wakati wa mechi ya nusu fainali ya kombe la FA kati ya Liverpool na Notingham Forest ambapo mashabiki 96 walikufa huku zaidi ya 700 wakijeruhiwa.Huu ulikua uwanja wa Sheffield Wednesday na ulitumika kama uwanja huru kwa ajili ya mechi hiyo.
Kwa miaka mingi mashabiki wa Manchester United wamekuwa wakiimba nyimbo za kashfa na pia kukejeli vifo hivyo katika masihara yao kabla na wakati wa mechi dhidi ya mashabiki wa Liverpool ambao tukio hilo liliwagusa sana.Kwa leo kwenye kumbukumbu hii kumekuwa na hamasa ya pande zote kusahau tofauti zao na pia kuheshimu marehemu hao katika kumbukumbu hii huku Sir Alex Ferguson akiandika barua ya wazi kwa mashabiki wa timu yake ya Manchester United kuwasihi waonyeshe heshma kwa marehemu na wote wanaokumbukwa leo kabla ya mechi yao pale Anfield.
Steven Gerrard ambaye ni nahodha wa Liverpool amezungumzia kuwapa heshima stahili mashabiki hao katika mechi ya leo na kusisitiza uzito wa mechi hii katika ulimwengu wa soka kwa kuiweka juu zaidi ya mechi ya Classico ya Hispania katika mazungumzo na waandishi wa habari katika maandalizi ya mechi hii.
Timu hizi zilitoka sare ya 1 - 1 mara ya mwisho kukutana Anfield Oktoba tarehe 15 mwaka jana na magoli yalifungwa na  Steven Gerrard na Javi Hernandez.Katika mechi kumi zilizopita kati yao Liverpool wameshinda mara 4 wakati Man Utd wameshinda mara 5 na kutoka suluhu mara 1.Ndani ya masaa 6 yajayo joto likipanda macho yetu wote yatakuwa Anfield kufuatilia pambano hili.May the best team win.

No comments:

Post a Comment